UVUMILIVU!

Wiki hii inayoisha nilibahatika kushirika Selous Marathon moja ya marathon zilizojizolea umaarufu sana hapa nchini kwa miaka ya karibuni.Safari hii nilichagua kukimbia mbio za milimani maarufu kama trail.Haikuwa rahisi hata kidogo lakini nashukuru niliweza kukamilisha mbio hizo na kupata medali yangu.

Tuachane na hilo sababu sio haswa dhumuni la makala hii fupi.Kipindi cha nyuma niliwahi kushirikisha juu ya mwanariadha wa Kitanzania John Akhwari ambaye alishiriki mashindano ya riadha nchini Mexico mwaka 1968.

Kwenye mbio zile za kilometa 42 kwa bahati mbaya sana wakati tu John anaanza alipata shida kwenye goti na mabegani.Hii ilitokana na hali ya hewa ya milimamilima iliyopo nchini Mexico.

Hilo halikuwa sababu ya John Akwar kuahirisha mbio hizo ambazo zilishuhudia idadi kubwa ya wanariadha kuishia njiani.

Waliofanikiwa kufika mwisho wa mbio walikuwa wameshapewa medali zao ila hadi giza linaanza kuingia ndipo alipoingia bwana John Akhwari.Watu waliokuwepo Uwanjani walimshangilia licha ya kuwa ndio alikuwa mtu wa mwisho kwenye mbio zile.

Kitu kikubwa ni pale mwandishi wa Habari alipomuhoji kwa nini hakuahirisha mbio zile pamoja na changamoto aliyoipata.Yeye alijibu ‘Nchi yangu haikunituma maili elfu tano Kuja hapa kuanza tu mbio,ilinituma maili elfu tano Kuja kumaliza mbio’.

Unaweza kuipata video kupitia YouTube.

Somo kubwa ambalo tunaweza kuondoka nalo hapo ni UVUMILIVU.Baada ya kujua nini haswa tunataka kwenye maisha yetu uvumilivu unahitajika sana.Sio kwenye fedha,biashara, kazi,mahusiano au maisha kiujumla uvumilivu unahitajika sana.

Kama kuna kitu kingine muhimu cha kuwafundisha watoto wetu basi ni UVUMILIVU.

Makala hii imeandikwa na Innocent Didas.

Mzazi,mtaalam wa malezi na mjasiriamali.

0764639570

Morogoro Tanzania.

Kuwa shabiki yao namba moja.

Kwa siku za karibuni ushabiki wa michezo na mambo mbalimbali umeongezeka kwa kiwango kikubwa sana.Angalia ushabiki kwenye mpira wa miguu,siasa,ngumi au mambo mengine.

Kama wazazi tunatumia muda wetu mwingi kwenye ushabiki wa mambo mbalimbali na tukasahau watu muhimu sana kwetu;watoto wetu.Ushabiki umekuwa hatari zaidi hasa kwenye zama zetu za mitandao ya kijamii.

Ushabiki kwenye mambo mbalimbali unatumia muda wetu mwingi na wakati mwingine fedha zetu nyingi huku tukiwasahau watoto wetu.

Kama ilivyo kwa michezo tunayoshabikia watoto wetu wanahitaji tuwashabikie kwenye mambo yao.Hii ni kutokana na ukweli kuwa watoto wetu kama walivyo watu wengine wanahitaji kuthaminiwa na kujaliwa.

Kwa kuwathamini na kuwajali watoto wetu tunawafanya kuwa marafiki zetu wa karibu.Pia kwa kuwa mashabiki wao wa kwanza tunawafanya watuamini na wawe tayari kutueleza mambo mbalimbali yanayowakabili.

Wakati mwingine watoto wetu wanaweza kuwa hawafanyi sawasawa na vile tunavyotegemea wafanye ila bado tunapaswa kuendelea kuwa mashabiki wao.Kama ilivyo kwa timu unayoipenda huachi kuwa shabiki kwa timu yako kufungwa ndivyo tunavyopaswa kuendelea kuwa mashabiki namba moja kwa watoto wetu.

Tusiwe aina ya wazazi ambao muda wetu mwingi tunatumia kuwaponda watoto wetu bali tutumie muda wetu na fedha zetu kuwa mashabiki kwa watoto wetu ili kuwasaidia kutumia uwezo mkubwa ulio ndani yao. Kwa kufanya hivyo tutawasaidia watoto wetu kujiamini zaidi na kufanya makubwa.

Makala hii imeandikwa na

Innocent Didas

Mzazi,mtaalamu wa malezi na mjasiriamali.

0764649570

Morogoro Tanzania

Huwezi kuutafuta mwiba uliokuchoma mguu wa kushoto kwenye mguu wa kulia.Funzo kubwa kwenye malezi na maisha.

Kama umewahi kuishi kijijini pengine umewahi kuchonwa na mwiba au kuona mtu aliyechomwa na mwiba.Leo nimekutana na funzo moja kutoka kwa mzee mmoja wa kipogoro juu ya kuchomwa na mwiba.

Unapochomwa na mwiba huna budi kuutafuta na kuutoa la sivyo utakusumbua.Lakini cha muhimu zaidi, sehemu mwiba ulipokuchoma ndipo haswa unapotakiwa kuutafuta na kuutoa.Huwezi kuchomwa na mwiba kwenye mguu wa kushoto halafu ukautafuta kwenye mguu wa kulia la hasha.Ni pale pale ulipokuchoma.

Msemo huu wa Kipogoro umenifanya kutafakari kwa kina vipi sisi wazazi tunaweza kuutumia kwenye malezi ya watoto wetu na maisha kiujumla.

Moja ya funzo kubwa nililoondoka nalo kutoka kwenye msemo huu ni kuwa ufumbuzi wa tatizo lolote lile unapunapaswa kufanyika pale pale kwenye tatizo na si mahali pengine.

Mfano wazazi mna matatizo ya kiuchumi halafu kutwa kucha mnakaa kulalamikia wengine sio suluhisho.Ni sawa na kuutafuta mwiba uliowachoma mguu wa kushoto kwenye mguu wa kulia.

Pengine ni migogoro kwenye familia kati ya wenza ambayo mnaona wazi inawaathiri watoto wenu;kuwashirikisha wengine badala ya kukaa chini wenyewe na kuitatua ni sawa na kuchomwa na mwiba mguu wa kushoto na kuutafuta kwenye mguu wa kulia.

Kwa tatizo lolote kwenye malezi au maisha kama familia suluhisho lijikite kwenye tatizo na wala si pengine; hapo ndipo tutakuwa tumeutafuta mwiba pale ulipotuchoma na wala si pengine.

Makala hii imeandikwa na

Innocent Didas

Mzazi,mtaalamu wa malezi na Mjasiriamali

0764639570

Morogoro,Tanzania

Uchambuzi wa Kitabu Zawadi kwa wanangu(A gift to my children).Ushauri wa baba kuhusu maisha na uwekezaji cha Jim Rogers

Kuwa mwananchi wa dunia.

Ni wazi kuwa watu wanabaguana kutokana na rangi,makabila au dini zao. Lakini unapochunguza sana unagundua kuwa watu wote ni sawa na tunapenda vitu sawasawa katika maisha.

Mwandishi anakumbuka alipokuwa anakuwa kwenye mji wao familia za watu weupe zilikuwa hazichangamani kabisa na familia za weusi. Ni hadi alipoenda kukaa na mjomba wako ambaye alikuwa akifanya biashara eneo la watu weusi.Siku moja alikutana na mwanamke wa Kijapani ambaye aliolewa na mtu mweusi.Hii ilimfanya kufikiria sana kwamba kumbe huyu mwanamke angeweza kuolewa na mtu mweupe na maisha yakaenda sawa tu.

Mwandishi anaeleza kuwa hata ukiangalia historia za vita utagundua kuwa vita nyingi zinatokea kutokana na utofauti ambao watu wanauweka mbele. Pia vita si kitu kizuri kabisa hata kwa nchi inayoshinda.Anashauri wanae kuwa wanapoona vita kwenye nchi waliyopo waondoke mara moja. Unapotembelea dunia na kukutana na watu ndipo utakapogundua kuwa yale watu wanayosema kuwahusu watu ni tofauti kabisa na uhalisia.

Uchambuzi huu umefanywa na

Innocent Didas

0764639570

Morogoro Tanzania

Uchambuzi wa Kitabu Zawadi kwa wanangu(A gift to my children).Ushauri wa baba kuhusu maisha na uwekezaji cha Jim Rogers

Ifanye Dunia mtizamo wako.Tembea maeneo tofauti kuiona Dunia.

Kutembea maeneo tofauti duniani na kukutana na watu tofauti kutabadili sana fikra zako. Usiishie tu kusoma kwenye vitabu nenda kaione Dunia ilivyo.

Unapotembelea Dunia usiende tu kwenye yale maeneo ya kitalii bali nenda kwa watu wa kawaida kabisa.Hapo utajifunza mengi ambayo yatabadili kabisa mtizamo wako.

Mwandishi anaeleza wazi kuwa yeye alifanikiwa kuzunguka mabara yote ya Dunia tena mara ya kwanza kwa pikipiki.Alichogundua ni kuwa binadamu wote tunafanana haijalishi tofauti za rangi,kabila,utaifa n.k.

Kupitia zoezi hili utaweza kujigundua binafsi nini nguvu na madhaifu yako.Itaibua pia udadisi ambao hukua nao na kukusaidia kuona yale mambo uliyokuwa ukidhani ni ya muhimu kumbe si muhimu kihivyo.

Itaendelea…

Uchambuzi huu umefanywa na

Innocent Didas

Mzazi,mtaalam wa malezi na mjasiriamali.

0764639570

Morogoro Tanzania